Ngozi

Kwa maana mengine ya neno hili linganisha ngozi (maana)

Ngozi ya mkono wa binadamu

Ngozi ni ganda la nje linalofunika mwili wa mnyama au binadamu. Aina mbalimbali huwa na aina za ngozi tofautitofauti kulingana na mazingira wanapoishi na ukoo wa spishi mbalimbali. Ni wanyama wa nusufaili ya vetebrata pekee wenye ngozi; wengine kama konokono, kaa au wadudu huwa na kiunzi nje si ngozi. Mamalia wote walio sehemu ya vetebrata huwa na nywele angalau chache kwenye ngozi yao.

Ngozi ikiondolewa mwilini na kushughulikiwa kwa kuikausha na kutia madawa mbalimbali inaweza kutunzwa na kutumiwa kwa kutengeneza viatu, nguo n.k.

Kazi za ngozi

  1. Kazi ya ngozi ni hasa kukinga sehemu za mwili dhidi ya athira za nje hasa dhidi ya vijidudu na michakati zinazoweza kusababisha ugonjwa.
  2. Ngozi inatunza unyevu au kiwango cha maji mwilini ni kinga dhidi ya kukauka.
  3. Ngozi ni kinga dhidi ya maji ya nje ambayo ingeyeyusha kemikali za seli na kuzitoa nje ya mwili.
  4. Ngozi ina uwezo wa kutawala halijoto ya mwili ama kwa kutoa joto la ziada kwenda nje au kuitunza ndani ya mwili. Ngozi ikijikaza inatunza joto, ikilegea inapanusha eneo la uso wake na kupunguza joto la ndani ya mwili.
  5. Ngozi huwa na neva nyingi ni kiungo muhimu wa kutambua dunia.
  6. Ngozi inasaidia kupumua yaani kupeleka oksijeni kwenye seli; kwa mwanadamu seli za ngozi yenyewe zinapata oksijeni kutoka nje moja kwa moja; kuna wanyama kadhaa ambao hawana mapafu wanapoka mahitaji yote ya oksijeni kupitia ngozi yao.

Muundo wa ngozi ya mamalia

Katika ngozi ya mamalia kuna sehemu ya mbili:

Ndani yake kuna kanda mbalimbali; sehemu ya chini ni kanda la kizazi ambako seli mpya zinazalishwa; jinsi zinavyosukumwa kuelekea nje zinakauka na mwishoni zifikia nje kabisa zinatoka kama mba.

Kanda za ngozi ya ndani zina hasa kazi ya kulisha na kushika epidemisi. Ndani yake kuna mishipa mingi ya damu na mishipa fahamu (neva). Ndani yake kuna pia tezi za jasho na tezi za mafuta. Kuna pia seli za musuli kwa ajili ya kukaza au kulegeza ngozi.

Rangi za ngozi

Rangi tofauti za ngozi zinategemea uwezo wa seli maalumu katika kanda la kizazi la epidemisi kutengeneza kiasi kikubwa au kidogo cha melanini.

Melanini ni rangi inayokaa ndani ya epidemisi yenye kazi ya kuzuia au angalau kupunguza athira za mnururisho wa jua. Mnururisho huo unaweza kuwa wa hatari kama jua ni kali na kuchoma seli, hasa kusababisha kansa.

Sehemu mbalimbali za mwili zinaweza kushika viwango tofautitofauti za melanini: ngozi ya makofi kwa kawaida ina melanini kidogo tu

Uwezo wa kutengeneza melanini unarithiwa. Hivyo watu "weusi" huzaliwa na kiwango kikubwa cha melanini ya kudumu kwenye ngozi. Watu "weupe" wana kiwango kidogo.

Katika mazingira yenye jua kidogo rangi nyeupe ina faida ya kwamba ngozi inahitaji nuru ya jua kwa kutengeneza vitamini D. Hapo mtu "mweusi" katika mazingira yenye jua kidogo anaweza kupata uhaba wa vitamini hiyo.

Kinyume chake wingi wa nuru inaongeza hatari ya kushika kansa ya ngozi. Watu wa Australia waliotoka katika koo za Wazungu wa Ulaya ilhali wanaishi katika nchi ya tropiki yenye jua kali wana kiwango kikubwa cha kansa ya ngozi.

Tabia hizo zimesababisha ya kwamba mara nyingi watu katika nchi za jua kali ni "weusi" zaidi lakini watu kwenye nchi za jua kidogo ni "weupe" zaidi maana tofauti za rangi ya ngozi zinasababisha faida au hasara za kiafya kulingana na mazingira.

Pale ambako hali ya jua ni ya katikati watu wa kila rangi wanaweza kuishi bila matata, lakini wakizaa pamoja kwa kawaida urithi wa ngozi nyeusi zaidi hushinda juu ya urithi wa rangi nyeupe.

Viungo vya nje

Wikimedia Commons ina media kuhusu:
Ngozi
Makala hii kuhusu mambo ya anatomia bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Ngozi kama matumizi yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.
This article is issued from Wikipedia - version of the 6/15/2016. The text is available under the Creative Commons Attribution/Share Alike but additional terms may apply for the media files.